Make your own free website on Tripod.com

TAARIFA YA HALMASHAURI YA WALEI PAROKIA YA UPANGA KWA KIPINDI KUANZIA MEI, 1998 HADI JUNI, 2001.

 

1.0 UTANGULIZI

 

Uchaguzi wa Halmashauri ya Walei na Kamati Tendaji ulifanyika sambamba na uanzishaji wa Jumuiya Ndogo Ndogo hapa Upanga. Kabla ya pale kulikuwa na Jumuiya moja tu, Jumuiya ya Mt. Yohani Mbatizaji. Aidha katika kipindi cha uhai wa Halmashauri hii, tulishuhudia na kushiriki katika tukio kuu na la maana sana katika historia ya Kanisa. Adhimisho la Jubilei Kuu ya miaka 2000 tangu kuzaliwa kwa mkombozi wetu, Yesu Kristo. Ni mapenzi au upendeleo wake Mwenyenzi Mungu ndio uliotufanya tujikute tukiongoza Parokia hii katika mwaka Mtakatifu. Hatuna budi kumshukuru Mungu kwa zawadi hii.

 

 

2.0 UCHAGUZI WA VIONGOZI, 1998

 

Halmashauri ya Walei inajumuisha Wenyeviti wote wa Jumuiya kumi na saba, Wenyeviti wa Vyama vya Kitume, yaani, Wawata, Viwawa, Moyo Mtakatifu wa Yesu na CPT; na mwisho wajumbe watano waliochaguliwa na Paroko. Kutokana na wajumbe hawa, wafuatao walichaguliwa kuingia katika Kamati Tendaji:

 

1.     Ndugu John B. Mwenda – Mwenyekiti.

2.     Ndugu Pantaleo Shirima – Makamu Mwenyekiti.

3.     Ndugu Augusta Fernandes – Katibu.

4.     Ndugu M. X. Kayombo – Katibu Msaidizi.

5.     Ndugu Salvatori Mushumbusi – Mweka Hazina.

 

Aidha wenyeviti na wajumbe walichaguliwa kuongoza kamati ndogo ndogo mbalimbali. Kwa jumla Halmashauri na Kamati zake mbalimbali walifanya kazi zao kwa ushirikiano na upendo. Katika kipindi chote cha miaka mitatu hapakuwa na mizozo yoyote. Mikutano yote iliendeshwa kwa utulivu na maoni ya kila mjumbe yalizingatiwa.

 

 

3.0 IDADI YA WAUMINI

 

Mpaka mwisho wa mwaka 1998 iliaminiwa kuwa Parokia ya Upanga ilikuwa na jumla ya waumini elfu nne na mia tano. Lakini baadaye ikaanza kuonekana upungufu katika mahudhurio hasa wakati wa ibada ya Jumapili. Pia kiasi cha michango ya kila Jumapili kilikuwa hakina uwiano hata kidogo na idadi hiyo ya waumini.

 

Kwa hiyo Halmashauri iliamua sensa ifanywe ili idadi halisi ijulikane. Kila Mwenyekiti wa Jumuiya alitakiwa atayarishe orodha ya waumini wote waliomo ndani ya eneo la Jumuiya yake. Zoezi hili lilifanyika na kukamilika mwisho wa mwezi Novemba, 2000. Sensa hii ilionyesha kwamba idadi halisi ya waumini katika Parokia hii ilikuwa elfu moja na mia tano, badala ya elfu nne na mia tano iliyokuwa ikidhaniwa hapo awali. Sababu ya msingi ya waumini kupungua hapa Upanga ni kwamba wengi wa waumini wanaishi katika nyumba za kupanga: walizopangishiwa na waajiri wao au walizopanga wao wenyewe, hasa kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Kwa hiyo wakitoka katika utumishi wa mwajiri inawabidi waache nyumba hizo na ni mara chache sana wakazi wapya ni wakatoliki. Kuhusu wapangaji wa NHC, hawa wakihama, nyumba zao kwa kawaida hupangishwa wahindi. Katika hali hiyo vijana wanapoamua kujitegemea huwalazimu kutafuta makazi nje ya Parokia ya Upanga. Mazingira ya namna hii hayasaidii kuongeza idadi ya waumini. Badala yake yana mwelekeo wa kupunguza idadi hiyo mwaka hadi mwaka.

 

 

4.0 MAPADRE NA WATAWA

4.1 Mapadre

 

Wakati Halmashauri inayomaliza muda wake ilipochagiliwa, Paroko alikuwa Padre Mario Maccarini ambaye yupo hadi sasa. Wakati huo msaidizi wake alikuwa Padre Zakeo Laarhoven. Lakini baada ya muda mfupi, alipewa uhamisho kwenda Parokia nyingine mnamo mwezi Machi, 1998. Hakuletwa Padre Msaidizi mwingine mpaka mwezi Machi, 2000 alipowasili Padre Silvano Nardi ambaye yupo nasi mpaka hivi sasa.

 

Katika kipindi hiki cha miaka mitatu, Baba Paroko na Wasaidizi wake wamefanya kazi nzuri sana, hususan katika kuziimarisha Jumuiya Ndogondogo za Kikristu ambazo zilianzishwa katikati ya mwaka 1998 sambamba na uchaguzi wa Halmashauri inayomaliza muda wake.

 

4.2 Masista

 

Masista wanne kati ya watano waliokuwepo wakati Uongozi unaomaliza muda wake unaingia madarakani baada ya muda walipewa uhamisho kwenda vituo vingine. Masista hawa ni Sista Angela Brigita, Sista Maria Rosa, Sista Maria Veneranda na Sista Maria Theresilia. Sista Maria Rosa Silvana alibaki na bado yupo. Masista waliochukua nafasi ya wale walioondoka ni Sista Maria Stella, Sista Maria Paskurina, Sista Laurensia Rosalia na Sista Maria Ludovika.

 

Baadhi ya kazi muhimu zinazofanywa na Masista ni kufundisha dini katika shule zilizomo ndani ya Parokia yetu; pia kuwaandaa watoto na watu wazima kwa Masakramenti mbali mbali. Aidha masista hawa wanawajibika kutoa huduma Kanisani kila siku, kuandaa chakula kwa mapadre na kufundisha katika shule zetu za chekechea na ushonaji. Kazi zote hizi wanazifanya kwa furaha na upendo. Tunawashukuru sana.

 

4.3 Mabruda

 

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, tumekuwa na Mabruda wawili. Kwanza alikuwepo Bruda Pius Nkilagomva. Huyu alipopelekwa Afrika ya Kusini, Bruda Giorgio alichukua nafasi yake kuanzia mwezi Oktoba, 1998. Moja ya shughuli ambazo walishughulikia ni kusimamia mambo ya vijana, kupokea wageni, kutoa huduma kwa maskini na pia kushughulikia masuala ya Procure ya Shirika.

 

 

5.0 UTOAJI WA MASAKRAMENTI

 

Katika kipindi kuanzia mwaka 1998 hadi 2000 idadi ya waumini waliopewa Masakraenti mbali mbali ni kama inavyoonyeshwa hapa chini:

 

Mwaka

Ubatizo

Komunio ya Kwanza

Kipaimara

Ndoa

1998

53

58

88

27

1999

66

71

111

18

2000

67

82

105

31

 

 

6.0 VYAMA VYA KITUME

 

Katika Parokia hii vipo Vyama vya Kitume Vitano: Wawata, Viwawa, CPT, Moyo Mtakatifu wa Yesu na Shikwaka.

 

6.1 WAWATA

 

WAWATA ni moja ya Vyama vya Kitume vinavyotegemewa sana hapa Parokiani. Ni moja ya mihimili inayoshikilia uhai wa Parokia yetu.

 

Tarehe 21 Aprili, 1999 WAWATA walipata pigo kubwa sana pale Mwenyezi Mungu alipoamua kumchukua kwake Mwenyekiti wao, Mama Elizabeth Massawe. Mwenyekiti mwingine hakuchaguliwa mpaka mwezi Agosti mwaka huo huo, alipochaguliwa Mama Dafrosa Tairo kama Mwenyekiti. Lakini miezi mitatu au minne baadaye alihamia Parokia nyingine. Kiti kilibaki wazi hadi tarehe 1.10.2000 alipochaguliwa Mama Adolphina Masaba kujaza nafasi hiyo. Katika wa hivi karibuni, Mama Masaba amechaguliwa tena kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

 

Pamoja na misukosuko iliyowapata, WAWATA waliendelea kwa nguvu moja na kazi yao ya kitume. Walishiriki katika kazi mbalimbali Parokiani, Jimboni mpaka Taifani; waliwatembelea wagonjwa; walishiriki kikamilifu katika masuala yote ya Adhimisho la Jubilei Kuu: Walishiriki katika Hija zote zilizowahusu huko Pugu na Bagamoyo na katika Jubilei mbalimbali.

 

WAWATA Parokia wanakabiliwa na matatizo kadhaa. Moja ya matatizo hayo ni uzito wa akina mama wengi kushiriki katika shughuli za WAWATA. Hatua iliyochukuliwa ya kuanzisha matawi katika Jumuiya  (JNNK) zote inatumainiwa kuongeza ushirikiano. Tunaamini pia uongozi uliochaguliwa hivi karibuni utaleta ufumbuzi kwa matatizo yanayokisibu chama hiki.

 

6.2 VIWAWA

 

Uongozi wa Viwawa uliomaliza muda wake mwezi Mei, ulichaguliwa mwezi Mei, 1998. Lakini baada ya muda mfupi, yalitokea matatizo kidogo na ikawa lazima Mwenyekiti, Ndugu Thomas Njau ajiuzuru. Badala yake alichaguliwa Ndugu Flavian Arbogasti, naye pia, kwa sababu fulani fulani akalazimika kuondoka kwenye uongozi. Nafasi yake ikachukuliwa na Ndugu Edwin Mwenda ambaye aliendelea kuwa Mwenyekiti mpaka siku ya uchaguzi wa hivi karibuni.

 

Kuna utata kidogo kuhusu kijana wa aina gani anastahili kuwa mwanachama wa VIWAWA. Baadhi ya vijana hususan wasiokuwa na kazi maalumu, wanadhani VIWAWA ni kwa ajili ya vijana wenye kazi maalumu; kwa hiyo wanasita kushiriki. Kuna umuhimu wa suala hili kufafanuliwa.

 

Pamoja na mapungufu na matatizo yaliyojitokeza, VIWAWA waliendelea kutimiza wajibu wao kwa kiwango cha kuridhisha ya kutosha. Wanachama wamekuwa wakishiriki vizuri katika mambo yote ya kiroho. Wamehudhuria semina mbalimbali, mafungo, matukio yote makubwa kama vile matukio yote ya Jubilei Kuu – hija na jubilei mbalimbali. Baadhi yao, kwa kupitia Neo katekumenato, walikwenda hija huko Israel. Aidha vijana hawa wametoa misaada mbalimbali kwenye hospitali, n.k.

 

Kwa upande wa maendeleo ya kimwili; VIWAWA hawakulala. Mwaka 1998 waliandaa matembezi ambayo yaliwaingizia zaidi ya Shs. 2,000,000/=. Walizitumia fedha hizi kuanzisha mradi wa kuazimisha turbai, viti na meza. Mradi unaendelea vizuri.

 

Aidha vijana wengi wamechukua fursa ya mikopo kutoka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kujipatia stadi za kazi na pia kuanzisha miradi midogo midogo ambayo inawasaidia kukidhi mahitaji yao.

 

 

 

6.3 CPT

 

Tawi la CPT Parokiani ni dogo kutokana na waumini kutoshiriki katika shughuli zake. Haieleweki sawa sawa kwa nini hali iko hivyo ikizingatiwa kuwa Upanga imejaa waumini wenye fani mbalimbali tena za kiwango cha juu. Uongozi wa CPT unatakiwa kufanya kazi ya ziada kuinadi CPT.

 

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, CPT imefanya kazi nzuri. Kwa mfano, imeshughulika na matayarisho yote ya kuanzisha Bima ya Atiman. Mwaka jana CPT iliandaa chakula cha jioni ambacho kiliingiza kiasi kinachokaribia Shs. 1,000,000/= kwa ajili ya kuanzisha Zahanati ndogo hapa Parokiani. CPT ingeweza kutekeleza mambo mengi kama waumini wengi zaidi wangejiunga nayo.

 

6.4 MOYO MTAKATIFU WA YESU

 

Chama hiki kimendoofika sana baada ya Mwenyekiti wake, Mama Mlipano, kuhamia Parokia nyingine. Sasa hivi kina wanachama watano au sita. Kwa hiyo mwaka huu haikuwezekana kufanya uchaguzi wa viongozi.

 

6.5 KWAYA-SHIKWAKA

 

Katika Parokia yetu tumekuwa na kwaya tano; tatu zikiwa katika Kanisa la Parokia na mbili zikiwa Betania na Muhimbili. Kazi iliyokuwa inatukabili ni kuziimarisha kwa hizi na kuunda muungano wa kwaya hizi Kiparokia. Kwa kiasi fulani tumeweza kuziimarisha kwaya hizi kwa maana ya kuongezeka kwa waimbaji. Kazi ya kuunda muungano yaani Shikwaka hapa Parokiani imekamilika na katika uchaguzi uliofanyika tarehe 8.6.2001 viongozi wafuatao walichaguliwa:-

 

1.     Nd. Benedict Ngassa - Mwenyekiti.

2.     Nd. Ernesta Chalamila - Makamu Mwenyekiti.

3.     Nd. Edith Ndokidemi - Katibu.

4.     Nd. Nelson Tiba - Katibu Msaidizi.

5.     Nd. Romana Swai - Mweka Hazina.                                    

 

 

7.0 JUMUIYA NDOGO NDOGO ZA KIKRISTU (JNNK)

 

Mpaka karibu katikati ya mwaka 1998 Parokia hii ilikuwa na Jumuiya ndogo ndogo moja tu; Jumuiya ya Mt. Yohani Mbatizaji. Uchaguzi wa viongozi wa Parokia uliofanyika mwezi Mei, 1998, ulikweda sambamba na kuanzishwa kwa Jumuiya Ndogo Ndogo kumi na sita, na kufanya jumla ya Jumuiya kumi na saba. Kila Jumuiya ilichagua viongozi watano, yaani, Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Katibu Msaidizi na Mweka Hazina. Kutokana na waumini wengi kuhama, ilibidi Jumuiya mbili (Mt. Augustino na Mt. Stefano) ziunganishwe na kufanya Jumuiya moja. Kwa hiyo sasa zipo Jumuiya 16.

 

Pamoja na kwamba wana-Upanga hawakuwa na uzoefu wa kutosha kuhusu uendeshaji wa jumuiya Ndogo Ndogo, lakini walijitahidi sana. Haikuchukua muda na Taasisi hizi zikachukua sura nzuri.

 

Katika kipindi hiki cha miaka mitatu iliyopita, Jumuiya zote zimejiwekea utaratibu wa vikao vya sala na vya kawaida. Zinatambua kuwa nia na madhumuni ya Jumuiya siyo kusali tu pamoja, bali pia ni kuishi pamoja; kusaidiana katika mambo ya kiroho na kimwili; katika raha na shida.

 

Jumuiya zote zinashiriki katika mambo yote ya kiparokia. Kwa mfano, Jumuiya zote zilitoa michango kwa ajili ya kumpongeza Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alipoteuliwa na Baba Mtakatifu kuwa Kardinali. Pia Jumuiya zote zilitoa michango ya kumpongeza Mhashamu Askofu Methodi Kilaini alipoteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dars es Salaam.

 

Ziara ya Bikira Maria katika Jumuiya inasaidia kuimarisha imani ya wana-jumuiya. Ziara ya Msalaba wa Jubilei katika Jumuiya zote ulileta msisimko wa kiimani ambao hautasaulika.

 

Jumuiya nyingi zimejiimarisha kifedha. Zinatumia akiba hizo kwa ajili ya tafrija mbalimbali, kusaidiana katika shida na kadha wa kadha.

 

Viongozi wa Jumuiya wanajitahidi kuwahamasisha na kuwahimiza wana-jumuiya wenzao watekeleze majukumu yao kwa Kanisa, kama vile kulipa zaka na michango mbalimbali. Pia wanasimamia utoaji wa Sakramenti mbalimbali kama Ubatizo, Kipaimara n.k.

Mwisho, kila Jumuiya kwa zamu inashughulikia masuala ya usafi wa Kanisa na mazingira yake siku ya Jumamosi na kutoa huduma zinazotakiwa Kanisani siku ya Jumapili.

 

Pamoja na mafanikio yaliyoorodheshwa hapo juu, Jumuiya karibu zote bado zinakabiliwa na matatizo mengi. Kwa mfano, wanaume wengi bado hawaudhurii vikao vya Jumuiya. Ni wanawake na watoto ndio wanaohudhuria kwa wingi zaidi. Jumuiya nyingi bado zina matatizo ya fedha. Lakini matatizo haya yasiwe sababu ya kukata tamaa. Yawe ni changamoto ya kuongeza jitihada.

 

 

8.0 JUMUIYA/VIKUNDI

8.1 Neo katekumenato

 

Neo katekumenato ni njia, si chama cha kitume. Ni njia inayomsaidia muumini kutambua maana halisi ya Ukristu. Ni njia ya imani inayolenga kumsaidia mwumini kuishi ubatizo wake na ukatoliki wake.

 

Hapa Parokiani zipo Jumuiya tatu zenye jumla ya wakrstu wapatao themanini, vijana kwa wazee. Wakristu hawa hawa wamo pia katika vyama, Jumuiya na Kamati mbalimbali. Hii inadhihirisha kwamba wao si chama wala hawakujitenga na wenzao. Aidha Neo Katikumenato wametoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani ya waumini.

 

8.2 Karismatiki

 

Kikundi cha kwanza cha Karismatiki kilianzia Don Bosco na kilikuwa kinatumia lugha ya Kiingereza, mwaka 1999. Wazalendo walipoongezeka katika kikundi hicho, waliamua kuanzisha kikundi cha Kiswahili hapa Parokiani. Kikundi hiki kina waumini thelathini hivi, ingawa baadhi yao siyo hai. Katika uchaguz uliofanyika tarehe 6.6.2001, waumini walichaguliwa kushika nyadhifa mbalimbali:

 

1.     Nd. Eugene Kiliwa –Mratibu.

2.     Nd. Clara Kanza – Makamu Mratibu.

3.     Ndugu Stella Gwao – Katibu.

4.     Nd. Methodia – Katibu Msaidizi

5.     Ng. Gaspar – Mweka Hazina.

6.     Nd. Stella Chale – Mlezi.

 

Lengo kuu la Karismatiki ni kuamsha Ukristo na hasa kufufua karama za Roho Mtakatifu ndani ya waumini. Wana-karismastiki wanazingatia sana unyenyekevu na utii kwa uongozi wa mahalia. Wana-karismatiki hutumia njia mbili kuamsha Ukristo. Kwanza ni budi wajiamshe wao wenyewe, na pili wawaamshe wengine kwa kupitia Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo. Huduma kuu wanayotoa ni kuwaombea watu wote wenye shida.

 

 

9.0 HUDUMA ZA KIJAMII

 

Parokia inatoa huduma mbalimbali katika nyanja za elimu, afya na hifadhi ya jamii.

 

9.1 Shule ya chekechea

 

Shule hii ni ya siku nyingi. Lakini kwa muda fulani umaarufu wake ulipungua kidogo. Kwa hiyo Kamati ya shule ya chekechea, ambayo iko chini ya Halmashauri, ilifanya maamuzi matatu muhimu ili kuipa shule hii uhai mpya. Kwanza, majengo na vifaa vya kuchezea vilikarabatiwa. Fedha za kukarabati zilitolewa na wahisani, ambao tunawashukuru sana. Pili, Kamati iliamua watoto wafundishwe Kiingereza na pale inapowezekana wafundishwe kwa lugha hiyo. Mwisho, ada ilipandishwa kutoka Shs. 3,000/= kwa mwezi hadi Shs. 10,000 kwa mwezi, hatua ambao iliipa shule uwezo wa kuwalipa walimu mishahara mizuri zaidi. Tunafurahi kusema kuwa hatua hizo zimeonyesha mafanikio. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa kiwango cha kuridhisha. Hata hivyo jitihada zaidi zinatakiwa kuiboresha shule hii ambayo ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi wengi zaidi.

 

Tunamshukuru Mkuu wa shule, Sista Maria Rosa Silvana na walimu wenzake kwa kazi nzuri waliyofanya kwa kipindi hiki cha miaka mitatu iliyopita. Mungu awabariki.

 

9.2 Shule ya ushonaji

 

Shule hii ilijengwa kwa msaada wa wahisani kutoka Italia. Ilifunguliwa mwanzo wa mwaka 1999 ikiwa na darasa moja na cherehani

 

Hivi majuzi kwa msaada tena wa wahisani, shule imepanuliwa. Sasa ina madarasa mawili, ofisi na stoo. Ina walimu watatu na jumla ya wanafunzi 25. Tunachukua nafasi hii kumshukuru sana Baba Paroko, Padre Mario Meccarini kwa kuwa misaada hii ilipatikana kutokana na juhudi zake.

 

9.3 Mfuko wa Maendeleo ya Vijana

 

Mfuko huu unaendelea kupanuka na vijana wanazidi kunufaika. Hadi kufikia mwezi huu wa Juni, tutakuwa tumetumia kiasi cha

Shs 8,000,000 kwa ajili ya kuwakopesha au kuwasaidia vijana wetu kwa kuwalipia ada za shule au kwa kuanzisha miradi ya kujitegemea. Vijana wapatao hamsini wamepata msaada kutoka mfuko huu na baadhi yao sasa wanaendesha miradi yao wakijitegemea k.m. wanafanya useremala, welding, ufugaji, biashara ya duka n.k. na tunawafuatilia ili warudishe mikopo kama walivyoahidi.

 

9.4 Misaada kwa Maskini

 

Huduma hii imekuwepo siku nyingi, na kwa sasa inasimamiwa na Bruda George. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita waumini wametoa jumla ya Shs. 5,337,405/= kwa njia ya mchango wa pili Jumapili moja kwa mwezi kwa ajili ya huduma hii.

 

9.5 Kamati ya Matendo ya Huruma

 

Kamati ya Matendo ya Huruma ni moja ya matunda ya Jubilei Kuu ya miak 2000 tangu kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristu. Iliundwa na Halmashauri ya Walei ya Parokia kutokana na pendekezo la Halmashauri ya Decania ya Mtakatifu Yosefu yenye kujumuisha Parokia saba ikiwemo hii ya Upanga. Halmashauri ya Decania ilipendekeza kuwa kila Parokia itoe huduma ya hali na mali kwenye Taasisi angalau moja kwa watu wenye shida za msingi. Parokia yetu iliamua kutoa huduma kwa wagonjwa fukara katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 

Kamati ya Matendo ya Huruma ina wajumbe sita walioteuliwa na Halmashauri ya Walei ya Parokia yetu:

 

1.        Ndugu Martina Marmo – Mwenyekiti

2.        Ndugu Zestha Lyimo – Katibu.

3.        Bruda George – Mweka Hazina.

4.        Ndugu Katarina Lutayangilwa – Mjumbe.

5.        Ndugu Glen Dias – Mjumbe.

6.        Ndugu Joseph Mlay – Mjumbe.

 

Wito wa Halmashauri ya Parokia wa wakuwaomba waumini wachangie kazi ya Kamati hii ilipokewa kwa mikono miwili na wana-parokia wote. Iliamuliwa kuwa mchango wa pili wa Jumapili moja kila mwezi uwe kwa makusudi haya. Ni kitu cha kutia faraja sana kwamba wana-parokia wameonyesha ukarimu wa hali ya juu sana. Aidha waumini binafsi wametoa michango ya ziada kama ripoti ya fedha inavyoonyesha hapa chini:

 

maelezo

mapato

matumizi

·        Michango ya Kanisani

Tshs 2,360,120

 

·        Misaada kutoka kwa

Watu mbalimbali

 

Tshs 274,600

 

·        Matumizi ya vifaa mbalimbali, usafiri, n.k

 

 

Tshs. 1,365,870

·        Alibaki

 

Tshs. 1,268,850

 

Tshs 2,634,720

Tshs. 2,634,720

 

Utafiti wa Kamati ulibaini kuwa mahitaji ya wagonjwa fukara yalikuwa madogo madogo lakini ya lazima, kama vile sabuni, dawa za meno, mafuta ya kujipaka, maternity pads, karanga, matunda, maziwa kwa watoto. Wagonjwa wa ukoma wanaoishi katika wodi 25 walipewa sukari, mabeseni ya kunawishia vidonda, betri kwa ajili ya redio yao, mpira wa kumwagilia maj, majembe n.k. kwa ajili ya kutumia kwenye bustani yao ya mboga.

 

Licha ya misaada ya vitu, pia Kamati ilitoa fedha kuwawezesha wagonjwa kupata huduma mbalimbali kama vile, x-ray, dawa na usafiri kwa wagonjwa ambao baada ya kutibiwa hawakuwa na fedha za nauli kurudi makwao.

 

Kesi ya aina yake ambayo Kamati ya Matendo ya Huruma ilikumbana nayo inahusu msichana Lucy aliyekuwa amejifungua mapacha walioungana. Ilikuwa lazima wapelekwe Afrika ya Kusini lakini mzazi hakuwa na fedha za kununulia “Passport” na mahitaji mengine madogo madogo. Hivyo Kamati ilimpa msaada uliotakiwa na akaenda Afrika ya Kusini ambako watoto walitenganishwa na kurejea Dar es Salaam. Kamati bado inafuatilia maendeleo ya mapacha hawa pamoja na mama yao. Kwa kweli Kamati imefanya kazi nzuri sana na inastahili pongezi.

 

9.6 Zahanati Ndogo kwa Ajili ya Maskini

 

Uzoefu wetu katika kutoa misaada kwa masikini umeonyesha kuwa ndugu hawa, licha ya chakula na mavazi, wanahitaji pia matibabu. Sera ya uchangiaji wa gharama za matibabu katika hospitali za serikali imewafanya watu kama hawa washindwe kumudu gharama hizi. Kwa kuzingatia hali hii, Halmashauri iliazimia kuanzisha zahanati ndogo. Mradi huu unasimamiwa na CPT. Harakati za kuchangisha zilifanyika mwaka juzi na mwaka jana. Juhudi zaidi zinatakiwa

 

9.7 Bima ya Afya ya Catiman

 

Sera ya Serikali ya uchangiaji wa gharama za matibabu katika hospitali za Serikali inawatatiza siyo tu maskini bali hata watu wengine. Katika hali hii, Halmashauri ilikubaliana na ushauri uliotolewa na Padre Vic Missiaen kutoka Baraza la maaskofu Tanzania na kuanzisha mpango wa Bima ya Afya ya Catiman. CPT Parokia walipewa jukumu la kufuatilia suala hili. Walifanya hivyo na kukamilisha hatua zote mpaka hatua ya uandikishaji wa wanachama. Hadi sasa wanachama zaidi ya mia mbili wamekwisha kujiandikisha. Kilichobaki sasa ni kuitisha kikao cha waliojiandikisha ili wachague viongozi wao na mpango uanze. Uongozi mpya unaombwa ufuatilie suala hili muhimu.

 

9.8 Elimu ya Afya kwa Jamii

 

Watu wengi tunaamini kwamba baadhi ya maradhi yanaweza kuzuiwa kwa elimu ya afya. Mtu akijua jinsi gani ugonjwa unavyoweza kumwambukiza, ni rahisi kwake kuchukua tahadhari. Magonjwa ya zinaa, kwa mfano, yanaepukika iwapo watu wataelimishwa ipasavyo.

 

Idara ya Afya ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam imekuwa ikizihimiza Parokia zote ziunde Kamati za Elimu ya Afya kwa Jamii zitakazoratibu zoezi hili.

 

Suala hili liliwahi kufikishwa kwenye vikao vya Halmashauri. Baada ya kusitasita Halmashauri iliona suala hili la Elimu ya Afya kwa Jamii wakabidhiwe CPT kwa utekelezaji. Lakini CPT wamesema hawana uwezo wa kutosha wa kulitekeleza na hivyo kulirejesha kwenye Halmashauri ya Parokia.

 

Elimu ya Afya kwa Jamii ni kitu muhimu sana. Kwa hiyo uongozi unashauriwa kufanya kila liwezalo kulifanikisha jambo hili.

 

 

10.0 JUBILEI KUU 2000

 

Adhimisho la Jubilei Kuu 2000 ilitanguliwa na miaka mitatu ya maandalizi. Waamini wote Jimboni wakiwemo wana-upanga walijiandaa kwa namna mbalimbali kama vile kuhudhuria semina na mafungo.

 

Adhimisho lenyewe lilikuwa na matukio mbalimbali. Kulikuwa na Jubilei za makundi mbalimbali. Vivyo hivyo Hija kwenda Pugu, Msimbazi na Bagamoyo zilipangwa vizuri ilimradi kila kikundi kilipewa nafasi ya kujipatia neema na baraka katika mwaka huo Mtakatifu.

 

Ziara ya Msalaba wa Jubilei katika Parokia mbalimbali lilikuwa tukio lililosisimua sana. Sisi wana-upanga ni kama tulipendelewa sana maana tulikuwa miongoni mwa Parokia chache zilizobahatika kuusindikiza Msalaba kwend Kanisa Kuu la Mt. Yosefu baada ya kuzinduliwa kwake katika Kanisa la Mt. Petro, Oyster Bay siku ya Krismasi, 1999. Pia baada ya Msalaba kuzunguka katika Parokia, uliwasili Parokiani kwetu na tukawa nao siku ya Krismasi 2000 na mwaka mpya 2001. Msalaba ulizunguka katika Jumuiya zote kumi na saba ambako kulikuwa na shangwe na ibada mbalimbali. Tarehe 5 Januari tuliusindikiza kwa maandamano makubwa yaliyoongozwa na Mwashamu Askofu Methodi Kilaini hadi Kanisa kuu la Mt. Yosefu ambako maandamano yalipokelewa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Baadaye Mwadhama alifunga rasmi Adhimisho la Jubilei Kuu 2000.

 

11.0 SHEREHE NYINGINE

11.1 Kumpongeza Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo

Mwezi Novemba, 1998 ilifanyika Sherehe kubwa kumpongeza Mwadhama Kardinali Pengo kwa kuteuliwa kwake kuwa Kardinali. Pamoja na shangwe na vifijo, Jumuiya zote kumi na saba zilijitokeza kumpongeza Mwadhama na kumtunuku zawadi mbali mbali.

 

11.2 Sikukuu ya Familia na Mavuno

 

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, tumeweza kusherehekea sikukuu ya Familia na Mavuno mara mbili, yaani Juni 1999 na 3 Juni, 2001. Nia na madhumuni ya sikukuu hii ilikuwa kumshukuru kwa mema mengi aliyotujalia Mungu, na pia kutupa nafasi ya kutafakari umuhimu na utakatifu wa Taasisi ya Familia. Aidha tulichukua fursa hiyo kuchangisha fedha kwa makusudi mbali mbali.

 

11.3 Kutangazwa kwa mwenye Rehema Josephina Bakhita kuwa Mtakatifu.

 

Tarehe 1 Oktoba, 2000 Baba Mtakatifu, Yohane Paulo II alimtangaza Josephina Bakhita kuwa Mtakatifu. Kwa vile Masista wa Shirika alilolitumikia lina makazi yake hapa Upanga, Masista hao waliamua kutushirikisha katika Misa ya Shukrani iliyofuatiwa na sherehe kwenye viwanja vya Kanisa.

 

12.0 MUHTASARI WA MAPATO NA MATUMIZI 1998 – 2000

 

Mapato ya Parokia yanatokana na sadaka, michango mbalimbali, zaka na misaada kutoka kwa wahisani. Ufuatao ni muhtasari wa mapato na matumizi kwa kipindi kutoka 1998 hadi 2000:

 

mwaka

mapato

matumizi

1998

71,108,470

69,508,420

1999

74,478,812

68,794,817

2000

53,785,925